Rais William Ruto ameagiza kutathminiwa upya kwa ada ya shilingi milioni 3.2 ya kuondoa mizigo ya pamoja bandarini kufuatia maandamano ya wafanyabiashara wadogo.
Kiongozi wa nchi amependekeza bidhaa za thamani kubwa zitenganishwe na mizigo ya kawaida.
Akizungumza katika mkutano na wamiliki wa biashara wa ndogo na za kadri katika Ikulu ya Nairobi Jumatano, Ruto alisema serikali iko tayari kushughulikia malalamiko kuhusu kuongezwa kwa kiwango cha ada ya kuondoa mizigo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Wakenya wote wanapaswa kulipa kodi ili kusaidia kugharamia shughuli za serikali.
Rais aliagiza kwamba kontena zenye bidhaa za kawaida ziendelee kulipia ada ya shilingi milioni 2, huku zile zenye bidhaa za thamani kubwa zikikaguliwa zaidi na ada kuamuliwa kulingana na thamani ya bidhaa zilizomo.
“Kama kuna bidhaa za bei ghali, zitolewe kwanza. Kontena ambayo haina bidhaa za thamani kubwa, tuendelee na bei ya zamani. Zile zenye bidhaa za thamani kubwa lazima ijulikane ni bidhaa gani,” alisema Rais.
Rais Ruto alihoji iwapo kiwango kimoja cha ada ya kuondoa mizigo kinapaswa kutumika kwa kontena zenye bidhaa za thamani tofauti kwa kiasi kikubwa.
Ruto pia aliagiza Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Nchini, KRA kuwapatia wafanyabiashara orodha ya bidhaa za thamani kubwa ambazo hazitastahiki mpango wa ujumuishaji wa mizigo.
Aidha, Rais alitaka uwepo wa uwazi zaidi katika biashara ya ujumuishaji wa mizigo akiagiza KRA kuanzisha sajili rasmi ya mawakala wanaounganisha mizigo pamoja na wafanyabiashara ambao mizigo yao wanahudumia.