Mwanamuziki Spice wa Jamaica afurahia maisha Kampala

Aliamua kuacha gari na kuabiri boda boda jijini kampala kama njia ya kuhisi ulivyo usafiri huo.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa asili ya Jamaica Spice yuko jijini Kampala nchini Uganda ambapo anaonekana kufurahia mitindo ya maisha ya watu wa jiji hilo.

Spice ambaye yuko huko kwa ajili ya tamasha, alichapisha video inayomwonyesha akiwa amebebwa kwa pikipiki ya uchukuzi wa abiria almaarufu boda boda.

Aliandika, “Nchini Uganda hivi ndivyo wanasafiri haraka na leo nimedondoka kwenye gari langu na kuabiri pikipiki kuhisi inavyokuwa.”

Walinzi wake wanaonekana kukwazika na hatua hiyo lakini mrembo huyo anasema kundi lake lote lilishuka kwenye magari, wote wakaabiri boda boda kama yeye.

Nyota huyo wa mtindo wa Dancehall wa Jamaica ataandaa tamasha yake Mei 9, 2026, katika uwanja wa mchezo wa Kriketi wa Lugogo jijini Kampala.

Mwaka jana tamasha yake jijini Kampala ilifutiliwa mbali hali iliyoghadhabisha mashabiki lakini aliwaomba msamaha, huku akiahidi onyesho la kipekee Jumamosi.

Msanii huyo anaendelea kufurahia chakula, utamaduni, makaribisho na nguvu ya watu wa Uganda hususan wakazi wa Kampala anapojiandaa kuwatumbuiza.

Atakuwa jukwaani na wasanii tajika wa kike nchini Uganda kama vile winnie Nwagi, Cindy Sanyu na Karole Kasita kati ya wengine wengi.

Share This Article