Nyota wa zamani wa klabu ya Chelsea F.C. na Timu ya Taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, amekutana na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dodoma.
Drogba ambaye amekuwa nchini Tanzania tangu Mei 3, 2026, alikuwa ameandamana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda aliyemwalika nchini humo.
Mkutano huo unachukuliwa kuwa sehemu ya mipango ya kuimarisha diplomasia ya michezo, ambapo ushirikiano kati ya serikali na nyota wa kimataifa unatumika kukuza sekta ya michezo kama kichocheo cha ajira, uwekezaji na utalii wa michezo nchini.
Makonda alikuwa amemwalika Drogba kuwa mgeni wake rasmi wa kimataifa wakati wa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake bungeni, akiwa pia na wasanii na wanamichezo tajika wa Tanzania.
Waziri huyo aliwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ya mwaka wa kifedha wa 2026/2027 bungeni Mei 4, 2026.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano na Rais, Drogba alisema kwamba anafurahia kuchaguliwa kusaidia Tanzania kuendeleza tasnia ya michezo ambayo anasema inakua kwa kasi sana.
Mwanasoka huyo mstaafu alisema pia kwamba alifurahia kuona kwamba bajeti ya michezo nchini tanzania imeongezeka kutoka milioni 12 hadi zaidi ya shilingi milioni 200.
Jingine alilojukumiwa nyota huyo ni kusaidia taifa hilo la Afrika Mashariki katika maandalizi ya mashindano ya AFCON mwaka 2027, ambayo yanaandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania.