Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP Renson Ingonga ameelezea dhamira ya ofisi yake kufanya kazi na taasisi za uchaguzi, usalama na sekta ya haki kuhakikisha mchakato wa uchaguzi wa amani, wenye uwazi na wa kikatiba kuelekea 2027.
Amesema kuhakikisha uchaguzi wa kuaminika kunahitaji hatua iliyoratibiwa inayofanywa na taasisi zote zilizo na majukumu ya kutekeleza katika mfumoikolojia wa uchaguzi na haki.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa mashauriano ya ngazi ya juu uliofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi leo Jumatano.
Ingonga aliongeza kuwa viwango vya kikatiba vinavyoongoza uchaguzi vinatoa mpango bayana wa kitaifa, akitoa mfano wa Kifungu cha 81 cha Katiba kinachohitaji mfumo wa uchaguzi kutoa hakikisho la uchaguzi huru na wa haki.
Isitoshe, uchaguzi huo unapaswa kuwa ule usio na vurugu, matishio, ushawishi usiofaa na ufisadi.
“Utekelezaji wa madaraka haya unahitaji msaada kamili na ulioratibiwa kutoka kwa wadau wote wa sekta za usalama na haki,” alishauri DPP.