Polisi wapata mifugo 24 walioibwa kaunti ya Meru

Tom Mathinji
1 Min Read
polisi wapata mifugo 24 waliokuwa wameibwa kaunti ya Meru.

Maafisa kutoka asasi mbali mbali za usalama wanaohudumu chini ya operesheni ya Maliza Uhalifu, wamefanikiwa kuwapata mifugo 24 waliokuwa wameibwa katika kaunti ya Meru.

Polisi walipokea habari za kuibwa kwa mifugo kutoka eneo la Ntangilia, na wakaanzisha operesheni iliyowahusisha maafisa wa asasi mbali mbali, huku wakifuata njia ambazo mara nyingi hutumiwa na wezi wa mifugo

Huduma ya Taifa ya Polisi kupitia ukurasa wa X, ilisema maafisa wa usalama waliwafumania majambazi hao katika eneo la Chumvi, ambapo ufyetulianaji wa risasi ulishuhudiwa kati ya maafisa hao na wezi wa mifugo.

Polisi waliwashinda nguvu majambazi hao na kusababisha kupatikana kwa mifugo wote ambao walirejeshwa mikononi mwa mwenyewe katika kituo cha kibiashara cha Gambela.

“Operesheni hii inaashiria ufanisi wa juhudi za asasi mbali mbali za maafsa wa usalama chini ya Operesheni Maliza Uhalifu,” ilisema taarifa ya Huduma ya Taifa ya Polisi.

Huduma ya Polisi iliongeza kuwa operesheni hiyo inaendelea kuimarisha uwepo wa maafisa wa usalama na kusambaratisha mitandao ya wahalifu katika eneo hilo.

TAGGED:
Share This Article