Omollo: Umoja wa viongozi ni nguzo kuu ya maendeleo

Dr. Omollo alisema serikali imejitolea kuhakikisha maendeleo sawa katika maeneo yote ya nchi kupitia uwekezaji katika miundombinu, elimu,huduma za afya na utoaji huduma za umma.

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo.

Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, ametoa wito kwa viongozi wote kote nchini kushirikiana na kufanya kazi kwa umoja kwa manufaa ya wananchi.

Dkt. Omollo alisema uongozi jumuishi ni muhimu sana kufanikisha upatikanaji wa amani, kupiga jeki maendeleo na mshikamano wa kijamii.

Akizungumza kwenye ibada ya maombi na hafla ya kuchangisha fedha katika kanisa la Ogwedhi Seventh-day Adventist, eneo bunge la Suna Mashariki, kaunti ya Migori, Omollo alisema umoja miongoni mwa viongozi huchochea umoja miongoni mwa jamii na kubuni mazingira yanayotoa fursa kwa maendeleo kunawiri.

“Wakati viongozi wanadumisha umoja, wananchi pia wanakumbatia umoja. Wakati viongozi wanafanyakazi pamoja, jamii hunawiri. Makanisha yetu yanakuwa imara, taasisi zetu zinakuwa thabiti, na maendeleo yanawafikia watu wote kikamilifu,” alisema Katibu huyo.

Alidokeza kuwa wanasiasa wanajukumu la kuzika tofauti zao za kisiasa na kuangazia masuala yanayoboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo ambayo yameachwa nyuma kimaendeleo.

Omollo alisema serikali imejitolea kuhakikisha maendeleo sawa katika maeneo yote ya nchi kupitia uwekezaji katika miundombinu, elimu,huduma za afya na utoaji huduma za umma.

Alisema serikali imewekeza pakubwa katika miradi ya barabara, shule na huduma zingine za umma, ili kuimarisha maisha ya wananchi na kubuni fursa kwa vizazi vijavyo.

Share This Article