Mechi za mwisho hatua ya makundi kuwania Kombe la Dunia zitapigwa Jumamosi usiku huku ratiba kamili ya raundi ya 32 bora ikitarajiwa kubainika.
Uingereza na Panama watafungua ratiba ya kundi L kuanzia saa sita usiku wa manane uwanjani New Jersey mjini New York, Marekani.
Three Lions ya Uingereza ni sharti wapate ushindi ili kuwa na uhakika wa kuongoza kundi hilo.
Ghana-Black Stars watakuwa Philadelphia dhidi ya Croatia wanaohitaji sare ili kufuzu kwa raundi ya 32 bora.
Chui wa Congo watapimana nguvu na Uzbekistan katika kundi K saa nane unusu DRC wakihitaji ushindi kwa kila hali ili kufuzu kwa hatua ya 32.
Colombia na Ureno watashikana mashati katika mechi nyingine ya kundi K itakayochezwa sambamba kuanzia saa nane unusu usiku mshindi akimaliza kileleni.
Colombia wanaongoza kwa alama 6 mbili zaidi ya Ureno wanaokalia nafasi ya pili.
Saa kumi na moja alfajiri, ngoma itaelekea kundi J mabingwa watetezi Argentina wakikumbana na Jordan ambayo tayari imetimuliwa mashindanoni katika uchanjaa wa Dallas nao Algeria wapimane ubabe na Austria.