Idara ya mahakama yapendekeza kubuniwa kwa mahakama za matibabu na urejeshaji

Mahakama hizo maalum zilizopendekezwa zitazingatia mbinu ya kutatua changamoto kwa kushughulikia sababu za msingi zinazochangia mtu kutenda makosa,.

Marion Bosire
2 Min Read

Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama na Katibu wa Baraza la Kitaifa la Uratibu wa Utekelezaji wa Haki, NCAJ Winfridah Mokaya, jana aliwasilisha pendekezo la Idara ya Mahakama la kuanzisha Mahakama za Matibabu na Urejeshaji.

Aliwasilisha pendekezo hilo katika mkutano wa 38 wa Baraza hilo, ulioongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Mokaya alisema mahakama hizo maalum zilizopendekezwa zitazingatia mbinu ya kutatua changamoto kwa kushughulikia sababu za msingi zinazochangia mtu kutenda makosa, kama magonjwa ya akili, matumizi ya dawa za kulevya na changamoto nyingine za kitabia na kijamii, badala ya kuzingatia adhabu pekee.

Alibainisha kuwa Mahakama za Matibabu na Urejeshaji zitakutanisha majaji, waendesha mashtaka, mawakili wa utetezi, maafisa wa uangalizi wa wafungwa na wahalifu, wanaotoa huduma za matibabu, wataalamu wa ustawi wa jamii, na taasisi za kijamii ili kuandaa mipango ya urekebishaji inayozingatia mahitaji ya kila mtu.

Kupitia matibabu yaliyopangwa kwa utaratibu, usimamizi wa mara kwa mara wa mahakama na ufuatiliaji endelevu, mfumo huu unahamasisha uwajibikaji huku ukiunga mkono mchakato wa kupona na mabadiliko ya tabia.

Msajili Mkuu alisisitiza kuwa mfumo huo unaopendekezwa unalenga kupunguza kurudia kutenda makosa ya jinai, kuimarisha usalama wa umma, na kuendeleza utoaji wa haki ulio wa kibinadamu zaidi, wenye ufanisi, na unaomweka mwananchi katika kitovu chake.

Aidha, alipendekeza kuundwa kwa kamati ya taasisi mbalimbali ili kuandaa mfumo wa kuanzisha mahakama hizo maalum nchini Kenya, pendekezo ambalo lilipokelewa na kuungwa mkono na Baraza.

Share This Article