Zaidi ya raia 200 wa kigeni wakamatwa Uganda

Tom Mathinji
1 Min Read
Raia 231 wa kigeni wakamatwa Uganda.

Katika hatua inayoonekana ya kukabiliana na uhamiaji haramu nchini Uganda, raia 231 wa kigeni wamekatwa kwa kuingia nchini humo kinyume cha sheria.

Raia waliokamatwa ni kutoka Pakistan, Bangladesh, Ethiopia, India, Ghana, Myanmar, Sri Lanka, Malaysia na Cambodia.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uganda, raia hao wanaaminika kuwa wamekuwa wakijihusisha na shughuli za kutiliwa shaka nchini humo, na uchunguzi umeanzishwa kubaini uwepo wao nchini humo.

Msemaji wa Wizara hiyo Simon Peter Mundeyi, alidokeza kuwa baadhi ya raia hao walihadaiwa kuingia nchini humo kwa kisingizio watapata ajira. Hata hivyo baadhi ya wengine inasemekana wamehusika na uhalifu wa mtandaoni.

Aidha, wizara hiyo imeongeza kuwa huenda raia hao wa kigeni, ndio chanzo cha ongezeko la visa vya uhalifu wa mtandaoni nchini Uganda.

Mamlaka nchini Uganda ilisema ilipokea habari za kijasusi kuhusu idadi kubwa ya raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi Uganda, bila stakabadhi zozote.

“Wengi wao hawakuwa na pasipoti,” ilisema mamlaka nchini Uganda.

TAGGED:
Share This Article