Poghisio kugombea ugavana Pokot Magharibi mwaka 2027

radiotaifa
1 Min Read
Samuel Poghisio - Seneta wa zamani wa Pokot Magharibi

Seneta wa zamani wa kaunti ya Pokot Magharibi Samuel Poghisio ametangaza kuwa atagombea wadhifa wa ugavana kwenye kaunti hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Wadhifa huo kwa sasa unashikiliwa na Simon Kachapin.

Poghisio ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano anasema ana tajiriba ya kutosha aliyopata miaka kadhaa iliyopita kumbwaga Kachapin mwakani.

Ameahidi kuwa mtetezi wa amani, kuangamiza zimwi la ufisadi na kupanua uwezo wa kiuchumi wa kaunti hiyo.

Amelalamikia mitazamo hasi inayohusishwa na kaunti hiyo kama vile wizi wa ng’ombe, ukosefu wa usalama na kiangazi akiahidi kuwa utawala wake utafanya kila iwezalo kubadilisha mitazamo hiyo punde akiingia madarakani.

Gavana wa zamani wa kaunti hiyo Prof. John Lonyangapuo pia ametangaza kuwa atagombea wadhifa huo kwenye uchaguzi ujao.

Tangazo sawia limetolewa na mbunge wa Pokot Magharibi David Pkosing.

Taarifa ya Stephen Ayiengo

Share This Article