Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ugonjwa wa Ebola kuwa dharura katika mataifa ya Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) baada ya kuripotiwa kwa vifo 80.
WHO imesema kuwa ugonjwa wa Ebola ambao husababishwa na virusi vya Bundibugyo sio janga lakini mataifa yanayopakana na DRC yako katika hatari kubwa ya kuambukizwa.
Umoja wa Mataifa umesema kando na vifo 80 vilivyothibitishwa, kuna visa 246 ambavyo vimeripotiwa DRC baada ya uchunguzi wa maabara.
DRC imeripoti visa vya ugonjwa huo katika eneo la Bunia mkoani Ituri na kisa kingine kuripotiwa mjini Kinshasa.
Nchini Uganda kumeripotiwa vifo viwili kutokana na ugonjwa wa Ebola huku waathiriwa wakiwa abiria waliowasili kutoka DRC.