Lil Pazo asema hakuna anayepata pesa nyingi kutoka YouTube

Alisisitiza kuwa maonyesho ya moja kwa moja jukwaani ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwa wanamuziki.

Marion Bosire
2 Min Read
Lil Pazo

Msanii wa muziki nchini Uganda Lil Pazo amesema hakuna msanii wa Uganda anayepata fedha nyingi kupitia YouTube.

Badala yake, alisisitiza kuwa maonyesho ya moja kwa moja jukwaani ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwa wanamuziki.

Pazo amepuuza madai kwamba wasanii wa nchini humo wanapata mapato makubwa kupitia YouTube, akieleza kuwa fedha zinazotokana na jukwaa hilo ni kidogo zaidi kuliko vile watu wengi wanavyodhani.

Akizungumza kwenye mahojiano mwimbaji huyo alisema idadi ya watazamaji kwenye YouTube inaweza kuongeza umaarufu wa msanii lakini haimaanishi kuwa msanii huyo anapata mapato makubwa.

“Hakuna mwanamuziki wa Uganda anayepata fedha nyingi kupitia YouTube. YouTube ipo zaidi kwa ajili ya kujitangaza katika tasnia ya burudani. Fedha unazopata kutoka huko ni kidogo sana. Haziwezi kuendesha maisha ya muziki,” alisema msanii huyo.

Kwa mujibu wa Lil Pazo, wanamuziki hawapaswi kutegemea YouTube kama chanzo chao kikuu cha mapato, akieleza kuwa jukwaa hilo hulipa kiasi kidogo likilinganishwa na vyanzo vingine vya mapato.

Mwimbaji huyo alisisitiza kuwa maonyesho ya moja kwa moja bado ndiyo yanayoingiza fedha nyingi kwa wasanii wengi, na akawahimiza wanamuziki kujikita katika kupata nafasi nyingi za kutumbuiza badala ya kufuatilia tu ongezeko la watazamaji kwenye YouTube.

Kauli zake zimeongeza mjadala unaoendelea kuhusu mapato yanayotokana na huduma za kusambaza muziki kidijitali, huku wasanii kadhaa wa Uganda hivi karibuni wakihoji mchango wa majukwaa ya kidijitali katika mapato yao kwa ujumla.

Share This Article