Serikali imezipiga marufuku kampuni za kusaga miwa nchini dhidi ya kuagiza sukari kutoka ughaibuni.
Katibu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh anasema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba Kenya sasa inaweza kuzalisha sukari ya kutosha kukidhi mahitaji ya watu wake.
Alisema marufuku hiyo inakusudia kuwalinda wakulima wa miwa humu nchini, kuiboresha sekta ya sukari na kupunguza utegemezi wa sukari inayoagizwa.
“Kipaumbele chetu ni kulinda wakulima na kuhakikisha wanafaidika kutokana na bidii yao ya mchwa,” alisema Dkt. Kipronoh.
“Kenya sasa ina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha kukidhi mahitaji ya watu wake, na hakuna sababu ya kampuni zetu za kusaga miwa kuendelea kuagiza sukari wakati miwa bado haijavunwa nchini.”
Dkt. Ronoh aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kampasi ya 10 ya Shule ya Kilimo nchini Kenya katika eneo bunge la Seme, kaunti ya Kisumu.