Wasanii wa muziki wa Kenya, Bien, Nikita Kering, Njerae na Nameless, wameteuliwa kuwania Tuzo za African Muzik Magazine Awards,AFRIMMA mwaka 2026.
Uteuzi wa wasanii hao ni dhihirisho la kuendelea kuimarika kwa ushawishi wa Afrika Mashariki katika tasnia ya muziki barani Afrika. Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Septemba 12, jijini Dallas, Texas, Marekani.
Tanzania inaongoza kwa uwakilishi wa Afrika Mashariki mwaka huu, huku Juma Jux, Diamond Platnumz, Lavalava, Abigail Chams na Zuchu wakipata uteuzi katika vipengele mbalimbali. Kutoka Uganda, Eddy Kenzo pia ameingia kwenye orodha ya wasanii wa Afrika Mashariki walioteuliwa.
Wasanii hao wa ukanda huu wameungana na majina makubwa ya muziki barani Afrika, kama Davido, Burna Boy, Wizkid, Tems, Rema, Ayra Starr, Tyla, Asake, BNXN na Black Sherif, jambo linaloonyesha jinsi muziki wa Afrika unavyozidi kupata umaarufu na kukubalika duniani.
Uteuzi wa mwaka huu pia unaashiria kurejea kwa AFRIMMA baada ya miaka miwili.
Waandaaji wameupanua hafla hiyo na kuigeuza kuwa Tamasha ya Muziki ya AFRIMMA, itakayojumuisha maonyesho ya moja kwa moja ya wasanii, maonesho ya utamaduni na burudani mbalimbali za kipekee.
Mwanzilishi na Mtayarishaji Mkuu wa AFRIMMA, Anderson Obiagwu, alisema mapumziko hayo yaliwapa waandaaji fursa ya kuandaa tukio kubwa zaidi huku wakiendelea kutimiza dhamira yao ya kuendeleza muziki wa Afrika na kutambua vipaji bora vya wasanii wa bara hilo duniani.