Tanasha Donna amtembelea Zuchu na mwanawe

Tanasha ambaye yuko nchini Tanzania anasema haingekuwa vizuri aondoke bila kumwona.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Tanasha Donna ambaye ni mzazi mwenza wa Diamond Platnumz jana alimtembelea Zuchu aliyejifungua mtoto wa kike maajuzi na Diamond Platnumz.

Akizungumza na mwanahabari wa Wasafi Fm Juma Lokole kwa njia ya simu leo, Donna alielezea kwamba alikwenda kwa Zuchu na Diamond jana kumpongeza kwa kujifungua mtoto wa kike.

“Huyo mtoto ni dada ya mwanangu Naseeb Junior, kwa hivyo niliona ni vizuri niende nikamtembelee nimpe zawadi, nimpe pongezi, kwa sababu tuko hapa Tanzania haingekuwa vizuri niondoke bila kumwona,” alisema Tanasha.

Jana Jumapili Agosti 9, 2026, Tanasha alichapisha picha na video alizonakili akiwa nyumbani kwa Zuchu na nyingine inayoonyesha zawadi alizomletea mtoto zikiwa na barua kwa Naseeb yaani Diamond na Zuchu.

Kwenye picha hizo anaonekana dadake Diamond anayefahamika kama Esma, binti ya Esma na katika video aliyochapisha anaonekana akiwa na Zuchu akimpa kongole naye Zuchu akishukuru.

Awali kulikuwa na tetesi kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanamuziki hao wawili hawapatani kisa Diamond Platnumz ambaye wote wamekuwa na mahusiano naye nyakati tofauti.

Sasa dhana hiyo huenda imefutiliwa mbali.

Uhusiano wa kimapenzi kati ya Diamond na Tanasha ulikuwa wa mwaka 2018 na 2019, kabla yao kutengana mwanzo wa mwaka 2020. Mwanao, Naseeb Junior, alizaliwa tarehe Oktoba 2 2019, siku ambayo pia ni siku ya kuzaliwa ya babake.

Tangu wakati huo wawili hao wamekuwa wakishirikiana katika malezi ya mtoto huyo.

Share This Article