Lissu alalamikia kile anachokitaja kuwa kuharibiwa muda

Hii ni baada ya kesi inayomkabili kusimama kwa siku 166, tangu Februari 24, 2026, kutokana na hatua ya upande wa serikali kuwasilisha rufaa katika mahakama ya rufani

Marion Bosire
2 Min Read
Kiongozi wa chama cha CHADEMA Tundu Lissu

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha upunzani cha CHADEMA nchini Tanzania Tundu Lissu amelalamikia kile anachokitaja kuwa kuharibiwa muda na upande wa serikali katika kesi inayomkabili ya uhaini.

Lissu amerejea mahakamani leo kwa ajili ya kuendelea kwa kesi hiyo baada ya kusitishwa kwa siku 166 tangu Februari 24, 2026, kutokana na hatua ya upande wa serikali kuwasilisha rufaa.

Hatua hiyo ilichochewa na hatua ya Lissu ya kupinga vikali matumizi ya mashahidi wa siri katika kesi hiyo, ambapo mahakama ya rufaa ilikubaliana naye.

Kulingana naye, hatua ya upande wa serikali ililenga kumpotezea muda tu ili, “aendelee kukaa mahabusu”.

“Leo ni siku ya 166 tangu Februari 24 tangu mawakili wa serikali waende Mahakama yaRufaa na huko nikawashinda na sasa tumerudi Mahakama Kuu lakini tumerudi baada ya siku 166,” alisema Lissu mahakamani.

Picha na video zilizosambaa mitandaoni zilionyesha viongozi mbalimbali wa CHADEMA, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche wakiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es salaam kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao.

Ratiba ya mahakama kuhusu kesi hiyo inaonyesha kwamba sasa itaendelea kusikilizwa mfululizo hadi Septemba 7, 2026.

Lissu alikamatwa mara ya kwanza Aprili 9, 2025 kufuatia mkutano wa kisiasa wa amani huko Mbinga, kusini magharibi mwa Tanzania, ambapo aliongoza kampeni ya chama chake ya “No reforms No Election”.

Siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alishtakiwa rasmi kwa kosa la uhaini na kuchapisha taarifa za uongo.

Kesi hiyo ilianza rasmi Mei, 2025 kabla ya kusitishwa mwisho mwisho wa mwezi Februari kutokana na kesi hiyo ya rufaa.

Share This Article