Mkewe Rais azuru wanachama wa JOYWO Kisii na Nyamira

Anasema alishuhudia azma, ubunifu na ustahimilivu wa wanawake wanaotumia nguvu ya ushirikiano kuboresha maisha.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkewe Rais Mama Rachel Ruto amesisitiza kuhusu nafasi inayoongezeka ya biashara na shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na wanawake katika kubadilisha maisha ya familia na jamii.

Haya yanafuatia ziara yake kwa wanachama wa chama cha Joyful Women Organisation, JOYWO katika kaunti za Nyamira na Kisii.

Wakati wa ziara hizo, Bi. Ruto alisema alishuhudia azma, ubunifu na ustahimilivu wa wanawake wanaotumia nguvu ya ushirikiano kuboresha maisha yao na kujitengenezea fursa pamoja na familia zao.

Huko Nyamira, alisema wanawake wamegeuza kilimo cha ndizi na uongezaji thamani wa mazao kuwa biashara zinazozalisha kipato.

Juhudi hizo zinawawezesha wanachama kuvuka mipaka ya kilimo cha jadi kwa kutafuta njia mbalimbali za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Katika Kaunti jirani ya Kisii, wanawake wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi, zikiwemo kilimo, ufugaji wa kuku, utengenezaji wa matofali na biashara.

Hatua hizo zinaonyesha jinsi ujasiriamali wa ngazi ya chini unavyoweza kutengeneza vyanzo mbalimbali vya mapato.

Mama wa Taifa, ambaye ni mlezi wa Joyful Women Organisation, amekuwa akihimiza mfumo wa kukusanya na kuwekeza pesa katika shirika hilo kama njia ya kukuza ushirikishaji wa wanawake katika masuala ya kifedha na kuwawezesha kiuchumi.

Bi. Ruto alisema uzoefu wa wanawake katika kaunti hizo mbili umeonyesha uwezo wa ushirikiano katika kubadilisha miradi midogo kuwa fursa endelevu za kiuchumi.

“Hatua kwa hatua na Mama. Kote nchini,” alimalizia Mama Rachel akisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya taratibu yanayoanzia mashinani kote nchini.

Share This Article