Jaji Mkuu Martha Koome leo ameongoza uzinduzi wa mfumo mbadala wa kutatua migogoro katika kaunti ya Kisii, lengo likiwa kupanua ufikiaji wa haki.
Alizindua pia kituo cha kufanikisha mfumo huo pamoja na vituo vya usajili wa mfumo huo katika mahakama za mjini Kisii, Ogembo na Etago ambapo sasa wakazi watapata haki kupitia kwa mfumo unaoongozwa na jamii.
Koome alisema mfumo huo unaimarisha kujitolea kwa idara ya mahakama kutekeleza kifungu nambari 159 cha katiba kwa kupendekeza mfumo mbadala wa kutatua kesi kwa mujibu wa katiba, haki za binadamu na sheria.
Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati aliyehudhuria hafla hiyo alitaja hatua hiyo kuwa muhimu na ambayo inatekeleza maazimio ya kaunti ya kuhakikisha ufikiaji rahisi wa haki kupitia kuhusisha jamii.
“Ushirikiano kati ya kaunti yetu na idara ya mahakama utaleta mazuri mengi kwa watu wa Kisii katika utatuzi wa migogoro inayoweza kusuluhishwa haraka na kwa bei nafuu kupitia mfumo huu,” alisema Simba.
Joel Ngugi, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya utekelezaji wa mfumo mbadala wa utatuzi wa migogoro alisema, “Haki huanza punde tu watu wanapochagua mazungumzo badala ya malumbano”.
Kulingana naye haki ni kuhakikisha kwamba hata baada ya mgogoro kuisha, watu bado wanaweza kusalimiana, kushirikiana na kujenga maisha yao pamoja.
Jana wahusika wa idara ya mahakama na mfumo huo mbadala wa utatuzi wa migogoro waliuzindua katika kaunti ya Bomet.