Wazee wa vijiji watakiwa kuongoza mjadala wa maendeleo

Rais Ruto amesema mjadala unaopendekezwa kuhusu mkataba wa kitaifa wa maendeleo haupaswi kubaki katika ofisi za serikali au kumbi za mikutano pekee.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amewataka wazee wa vijiji kuongoza ushiriki wa wananchi katika mjadala unaopendekezwa kuhusu mkataba wa kitaifa wa maendeleo.

Akizungumza katika mkutano na wazee wa utawala wa vijiji katika Ikulu ya Nairobi, Ruto amesema mazungumzo hayo lazima yawafikie wananchi katika kila boma.

Mkataba huo unalenga kutafsiri ahadi za Katiba kuhusu huduma za afya, makazi bora, elimu, maji safi, usalama wa chakula na hifadhi ya jamii kuwa malengo ya kitaifa yanayoweza kupimwa.

Ruto alisema mjadala huo haupaswi kubaki katika ofisi za serikali au kumbi za mikutano pekee, bali unapaswa kuendeshwa hadi mashinani kupitia viongozi wa jamii wanaoaminika.

Aliwataka wazee wa vijiji kuwahamasisha wananchi kushiriki katika ajenda ya maendeleo ya serikali kwa kuhimiza uandikishaji wa watoto shuleni, upatikanaji wa huduma za afya, kilimo chenye tija, uhifadhi wa mazingira na kuishi kwa amani.

Kiongozi wa nchi alisema mafanikio ambayo Kenya imepata katika demokrasia yanapaswa sasa kuambatana na kuboreshwa kwa maisha ya wananchi na kupanuliwa kwa fursa za kiuchumi kwa wote.

Alisisitiza kuwa taifa halipaswi kuchagua kati ya demokrasia na maendeleo, akieleza kuwa yote mawili ni wajibu unaotokana na Katiba.

Alieleza kuwa wazee wa vijiji huwa daraja kati ya serikali na wananchi, na kuwataka kutambua familia zilizo katika mazingira magumu, kuzisaidia kupata huduma za umma na kuimarisha umoja katika jamii.

Aliwahimiza kuhakikisha hakuna kijiji kitakachosalia nyuma na kwamba kila Mkenya anashiriki na kunufaika na maendeleo na ustawi wa taifa.

Share This Article