Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga amesema afisi yake iko tayari kukabiliana na kesi zinazohusiana na uchaguzi, huku taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza kwenye kongamano la viongozi jijini Nairobi, Ingonga alisema afisi yake imebuni kitengo maalum ambacho kimejukumiwa kushughulikia kesi za kiuchaguzi, kikipigwa jeki na viongozi wa mashtaka waliopokea mafunzo kuhakikisha kesi hizo zinashughulikiwa kwa wakati unaofaa.
Ingonga aliwaonya wale wanaolenga kuvuruga mchakato wa uchaguzi kupitia ghasia, matamshi ya chuki, uhalifu wa mtandaoni, au uhalifu wa aina yoyote kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema afisi yake itashirikiana kwa karibu na wadau wengine ikiwa ni pamoja na asasi za uchunguzi, kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 unaandaliwa kwa mazingira ya amani, na wanaokiuka sheria za uchaguzi kuchukuliwa hatua.
Alidokeza kuwa sheria itatekelezwa kwa usawa bila ubaguzi, akisema maamuzi ya upande wa mashtaka hutekelezwa kwa njia huru kwa kuzingatia ushahidi uliopo.
Wengine waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na msemaji wa Huduma ya Taifa ya Polisi Muchiri Nyaga, mwenyekiti wa Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa Kasisi Kepha Omae, wanaharakati na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi miongoni mwa wengine.