Waakilishi wa Afrika Cape Verde na Misri, walizoa sare muhimu katika mechi za Jumatatu za Kombe la Dunia, linaloendelea nchini Mexico,Canada na Marekani.
Limbukeni Cape Verde maarufu kama Blue Sharks, walijizatiti na kulazimisha sare tasa dhidi ya ya mabingwa wa Ulaya Uhispania, uwanjani Mercedes Benz mjini Atlanta-Georgia.
Kipa wa Cape Verde Vozinha, alipangua takriban matobwe saba ya Uhispania na kutawazwa mchezaji bora.
Katika mechi ya pili ya kundi hilo Uruguay pia walitoka sare ya bao moja na Saudi Arabia.
Kundini G Misri wanaocheza Kombe la Dunia kwa mara ya nne waliwahemesha Ubelgiji uwanjani Seattle ,Mohamed Salah aliyekuwa akiadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa akimpokeza pasi Emam Ashour, aliyepachika bao la uongozi dakika ya 20 na kuongoza hadi mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Ubelgiji walikuwa na wakati mgumu na kusubiri hadi dakika ya 66, kabla ya nguvu mpya Romelu Lukaku kupiga shambulizi lililomkanganya beki wa Misri, Mohamed Hany na kujifunga.
Mechi ya baadaye ya kundi hilo pia ilimalizikia sare ya 2-2, kati ya Newzealand na Iran.