SHA imelipa shilingi bilioni 164 kwa vituo vya afya, asema Duale

Duale alisema kupitia mfumo wa Taifa Care, serikali imehakikisha Wakenya wanapata huduma za afya za ubora wa hali ya juu, bila kujali mapato yao, maeneo wanakoishi au hali zao za maisha.

Tom Mathinji
2 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya.

Waziri wa Afya Aden Duale ameelezea mafanikio makubwa yaliyonakiliwa katika wizara hiyo, huku Kenya inapojiandaa kwa kongamano la Afya mwaka 2026.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari Jijini Nairobi leo Jumanne, Duale alisema kupitia mfumo wa Taifa Care, serikali imehakikisha Wakenya wanapata huduma za afya za ubora wa hali ya juu, bila kujali mapato yao, maeneo wanakoishi au hali zao za maisha.

Duale alidokeza kuwa hadi kufikia sasa Wakenya milioni 31.2, wamesajiliwa kwa Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA), huku malipo milioni 7.9 yakishughulikiwa na takribani shilingi bilioni 164 zikilipwa kwa vituo mbali mbali vya afya.

“Wakenya waliosajiliwa kwa halmashauri ya SHA, wanaweza pata huduma za afya katika vituo vya afya vya Level 2, 3 na 4 kupitia hazina ya huduma ya afya ya msingi bila malipo,” alisema Duale.

Mary Muthoni – Katibu wa Afya ya Umma.

Wakati huo huo waziri huyo alisema wahamasishaji wa afya 107,000, wanaendelea kutoa huduma za afya ya msingi karibu na wananchi, akidokeza kuwa serikali pia inawekeza katika mpango wa kutenegeneza dawa, vifaa vya matibabu na miundombinu ya afya.

Akielezea mafanikio ya wizara yake, Duale alisema hivi majuzi serikali ilizindua kituo cha kitaifa cha ambulensi pamoja na nambari ya dharura ya 922 itakayofanikisha kupata huduma za afya bila kuzingatia eneo aliko mgonjwa au ikiwa amesajiliwa na SHA au la.

Dkt. Ouma Oluga – Katibu katika Wizara ya Afya.

Kongamano la Afya litaandaliwa kati ya Agosti 18-19 2026 katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), likileta pamoja Serikali ya Taifa, ile ya Kaunti, washirika wa maendeleo, taasisi za afya, sekta ya kibinafsi, wataalam wa afya na wananchi kukadiria na kupanga awamu ijati ya Huduma za Afya kwa Wote (UHC).

Wengine waliohudhuria mkutano huo ni Makatibu Dkt.  Ouma Oluga na Mary Muthoni, na Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt. Patrick Amoth miongoni mwa wengine.

Share This Article