Wakenya John Korir na Sharon Lokedi,ndio mabingwa wa makala 129, ya mbio za Boston Marathon zilizoandaliwa leo jioni nchini Marekani.
Lokedi ametwaa ubingwa wa kwanza wa mbio kuu, akiweka rekodi mpya ya saa 2 dakika 17 na sekunde 22 .
Lokedi aliyemaliza wa pili mwaka jana atapokea tuzo ya dola 50,000 kwa kuweka rekodi mpya.
Bingwa mara mbili wa mbio hizo Hellen Obiri, amemaliza wa pili kwa kutumia muda wa saa 2 dakika 17 na sekunde 41, huku Mwethiopia Yalemzerf Yehualaw, akiridhia nafasi ya tatu.
John Korir alitwaa ushindi wa mbio za wanaume akiziparakasa kwa saa 2 dakika 4 na sekunde 45, ukiwa ushindi wa pili baada ya kushinda London Marathon mwaka jana.
Felix Simbu wa Tanzania amemaliza wa pili kwa saa 2 dakika 5 na sekunde 4, huku Mkenya mwingine Cybrian Kotut, akishinda shaba kwa saa 2 dakika 5 na sekunde 4.
Mbio hizo ni za pili katika kalenda ya mbio saba kuu za marathon duniani na zitafuatwa na London Marathon Jumapili hii.