Mwigizaji wa Tanzania Wema Sepetu amesema kwamba kamwe hatojieleza kuhusu suala zima la iwapo kweli alibeba mimba na kujifungua.
Kupitia Instagram, dada huyo wa taifa la Tanzania alichapisha bango lenye maneno ya kuelezea hilo.
“Mtu aliniuliza, hautaelezea upande wako, nikajibu, mungu anajua na hilo linatosha” ndiyo maneno yaliyokuwa kwenye bango hilo.
Chapisho la Wema linachochewa na hatua ya watumiaji mitandao nchini Tanzania kutilia shaka ujauzito wake pamoja na kujifungua wengi wakihisi kwamba mwili wake haukuonyesha mabadiliko ambayo kawaida huja na ujauzito.
Awali alijirejelea kama tasa akiwataka wanaomsema wakome.
Wema Sepetu aliyewahi kuwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya ulimbwende amekuwa akijaribu kupata mtoto kwa muda mrefu na ombi lake lilitimia mwaka huu.
Alijifungua mtoto wa kiume aliyempa jina Ollie Juni 13, 2026 ambaye babake ni mwanamuziki mwenza na mpenzi wake Whozu.