Msanii wa muziki kutoka Nigeria Damini Ebunoluwa Ogulu maarufu kama Burna Boy, ameamua kuingilia tasnia ya filamu ambapo amefanya uzinduzi wa ulimwengu wa kazi yake mpya iitwayo “3 Cold Dishes”.
Uzinduzi huo uliandaliwa Oktoba 3, 2025 katika ukumbi wa Indigo ndani ya ukumbi mkubwa wa The 02, jijini London nchini Uingereza.
Akihutubia waliohudhuria uzinduzi huo, mamake Burna Boy Bose Ogulu ambaye pia ni meneja wake alisema wanaume wengi walikaribishwa katika ngono na waliowazidi umri ambao mara nyingi waliachwa nao kwa ajili ya kuwatunza.
Bose alisisitiza kwamba wanaume wengi walidhulumiwa kingono alipoangazia suala la ulanguzi wa binadamu na dhuluma mada zinazoanishwa kwenye filamu hiyo.
Filamu hiyo ya 3 Cold Dishes inahusisha wanawake watatu, mmoja kutoka Nigeria, mwingine kutoka Côte d’Ivoire na mwingine raia wa Benin wanaoungana tena miongo miwili, baada ya kuponea ulanguzi.
Lengo lao kuu wanapoungana tena ni kulipiza kisasi dhidi ya wanaume ambao waliwaharibia maisha yao awali.
Filamu hiyo iliyoandaliwa kwenye nchi kadhaa za Afrika Magharibi, inasimulia hadithi ya Esosa, Fatouma na Giselle, wanawake watatu waliolanguliwa wakiwa vijana na ambao walipata ujamaa katika machungu yao.
Wakiwa wamejihami na kiwewe, mkakati na kujitolea, watatu hao wanazindua oparesheni ya kuporomosha wanaume wenye ushawishi mkubwa waliowasababishia mateso.
Kinachoanza kama harakati ya kulipiza kisasi kinageuka kuwa safari ya kutafakari haki, utambulisho na kupona katika dunia ambayo haikutarajia kwamba wangeinuka.
3 Cold Dishes ni filamu mpya ya kusisimua inayovutia, iliyotayarishwa na Burna Boy kwa kushirikiana na Official Osas na The Namix, imeandikwa na Tomi Adesina na kuelekezwa na Surf.
Itaanza kuonyeshwa kwenye sinema mbali mbali ulimwenguni Novemba 7, 2025.
