Mbunge wa Murukweini aachiliwa huru kwa dhamana

Mbunge huyo anatuhumiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Kieni, kaunti ya Nyeri.

Martin Mwanje
2 Min Read
John Kaguchia - mbunge wa Mukurweini

Ni afueni kwa mbunge wa Mukurweini John Kaguchia baada ya kuachiliwa huru na mahakama kwa shilingi 250,000 pesa taslimu au dhamana ya shilingi milioni moja.

Mbunge huyo alibusu raha ya uhuru leo Jumatano alasiri wakati akisubiri kusomewa mashtaka hiyo kesho.

Awali, kulikuwa na ngonja ngoja nyingi mahakamani baada ya ripoti kuchipuka kuwa mbunge huyo hajulikani aliko.

Hali hiyo ilimlazimu Hakimu Theresa Nyangena kuvuta subira kwenye chumba chake hadi mshtakiwa ashushwe kizimbani.

Subira ambayo ilivuta heri kwani Kaguchia alijitokeza baadaye akiwa ameandamana na Seneta wa Nyandarua John Methu na mawakili wake.

Kaguchia alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jana Jumapili kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa eneo la Kieni, kaunti ya Nyeri.

Mbunge huyo alikamatwa baada ya kukesha usiku kucha katika afisi za chumba kimoja cha habari, alikoshiriki mahojiano.

Kaguchia, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua, amekuwa akimulikwa na vyombo vya usalama baada ya kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi wakati wa mkutano wa kisiasa Jumamosi iliyopita.

Ni matamshi yanayodaiwa kuwaonya wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kumpigia kura Rais William Ruto wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, Kaguchia amekanusha madai hayo akisema alinukuliwa vibaya.

Mbunge huyo alikamatwa wakati ambapo  Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano, NCIC inawachunguza baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa madai ya kutoa matamshi ya chuki.

Wanaochunguzwa ni pamoja na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na Mawaziri Aden Duale wa Afya na Geoffrey Ruku wa Utumishi wa Umma.

Share This Article