Kinara wa chama cha ODM Dkt. Oburu Oginga ametangaza kuwa yeye anatosha kuwa Naibu Rais wakati idadi ya wanaoemezea mate kiti hicho ikiendelea kuongezeka kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hata hivyo, Oburu amesema chama cha ODM hakitamsimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, bali kitamuunga mkono Rais William Ruto kuhudumu kwa muhula wa pili.
“Nyadhifa zingine zote zinaweza kujadiliwa. Hudhani nastahili kuwa namba mbili?” alisema Oburu katika hatua iliyovunja mbavu hadhira wakati akizungumza katika mkutano wa wazee wa vijiji ulioandaliwa katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.
“Si ninaweza kuwa namba mbili? Mimi nimetosha!”
Ingawa Oburu, ambaye pia ni Seneta wa Siaya, alitangaza tamanio lake mbele ya Rais Ruto, kiongozi wa taifa hakugusia hilo kwenye hotuba yake.
Chama cha ODM kimetangaza kuwa ingawa hakitamsimamisha mgombea wa urais, kingependa kukabidhiwa kiti cha Naibu Rais.
Ni matamanio ambayo yamepingwa vikali na viongozi kutoka Mlima Kenya wakiongozwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, wanaomshabikia Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki kuendelea kuhudumu katika wadhifa huo.
Wengine wanaoripotiwa kunyemelea wadhifa huo ni Mawaziri Hassan Joho wa Madini na Wycliffe Oparanya wa Vyama vya Ushirika.