PSC kuboresha sera ya PSIP ili kujumuisha wahitimu wa Diploma na TVET

Mwenyekiti wa PSC Francis Meja alisema hayo alipomzuru Waziri Wycliffe Oparanya.

Marion Bosire
2 Min Read

Tume ya Utumishi wa Umma, PSC imeanzisha mchakato wa kupitia upya Sera ya Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu katika Utumishi wa Umma, PSIP.

Lengo kuu la hatua hiyo ni kuwajumuisha wahitimu wa mipango ya mafunzo ya stashahada yaani Diploma na wale wa taasisi za Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Amali, TVET.

Haya yalitangazwa leo na mwenyekiti wa tume hiyo Francis Meja, wakati alimtembelea Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati, MSMEs Wycliffe Oparanya, katika Jengo la NSSF leo Agosti 4, 2026.

“Sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu kwa kile kinachotokea wakati wa utekelezaji wa mpango wa PSIP na baada ya wahitimu kuumaliza,” alisema Meja.

Aliongeza kusema kwamba mpango ulioboreshwa utashirikisha sekta ya kibinafsi, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, na kuanzisha mfumo wa kuweka akiba kwa wahitimu wanaoshiriki mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Oparanya alitoa wito wa kuanzishwa kwa mpango mmoja wa kitaifa wa mafunzo kwa vitendo wenye mfumo jumuishi wa kufuatilia maendeleo na utendaji wa kila mshiriki.

“Sote tunatumikia serikali moja. Mpango wa mafunzo kwa vitendo unapaswa kuratibiwa na kusimamiwa kwa pamoja ili kuhakikisha udhibiti wa ubora na uwepo wa viwango vinavyofanana,” alisema Waziri Oparanya.

Waziri huyo alimalizia kusema kwamba washiriki wote wa mafunzo hayo wanapaswa kupata manufaa yanayolingana bila ubaguzi.

Share This Article