Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kiprono Rono, amesema utoshelevu wa chakula nchini Kenya ndio usalama thabiti, huku akitoa wito kwa wanasayansi kuimarisha utafiti wao.
Akizungumza wakati wa kongamano la Kisayansi katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO) la mwaka 2026, Dkt Rono alitoa changamoto kwa wanasayansi kuhakikisha utafiti wao unawafaidi Wakenya wote.
Aliwataka wanasayansi hao kupanua utafiti wao na kuangazia zaidi maeneo kame, ambapo mabadiliko ya tabianchi yanaendela kuwa na athari hasi kwa maisha na uzalishaji wa chakula.
“Sayansi inapaswa kutoangazia tu maeneo 14 yanayozalisha chakula, lakini pia yaelekezwe katika maeneo kame,” alisema Dkt. Rono.
Wakati huo huo, katibu huyo alitoa wito kwa watafiti kubuni maarifa ambayo yatatumiwa katika sera ili kuchochea uvumbuzi unaozingatia mabadiliko ya tabia nchi kote nchini.
Dkt. Rono aliyasema hayo alipomwakilisha Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe kwenye hafla hiyo.