Gavana wa kaunti ya Kwale, Fatuma Achani, amezindua rasmi uchimbaji wa visima 28 vya maji vinavyotumia nguvu za miale ya jua au sola katika kaunti hiyo ya Kwale.
Uchimbaji wa visima hivyo unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti ya Kwale na Shirika la Kawi nchini la REREC.
Akizungumza katika kijiji cha Jeza eneo la Tsimba Golini huko Matuga kaunti ya Kwale katika uzinduzi huo, gavana wa kaunti hiyo Fatuma Achani amesema kuwa serikali yake hadi kufikia sasa imechimba Zaidi ya visima 100 na mabwawa 70 katika maeneo ya Matuga, Msambweni, Samburu, Kinango na Lungalunga mtawalia.
Achani aliongeza kuwa serikali yake itaendelea kuboresha miundo msingi ya maji katika kaunti hio ili kuona kuwa wakaazi wake wanapata maji ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, mifugo na kilimo nyunyizi.
Kulingana na Samuel Olela kutoka shirika la kawi la REREC shirika hilo la kiserikali litaendelea kushirikiana na serikali za kaunti katika uimarishaji ya miundo msingi ya maji nchini.
Wakaazi wa eneo hilo wakiongozwa na Omar Ramadhan,wamepongeza ujio wa mradi huo wa maji wakisema utawarahisishia upatikanaji wa bidhaa ya maji yaliyo safi na salama.