Shirika la Usafiri wa Meli la Tanzania (TASHICO) na kampuni ya usafiri wa majini ya Lignes ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), zimetia saini makubaliano ya miaka mitatu, kuboresha uchukuzi wa abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika, ili kufanikisha biashara na uunganishaji wa eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza katika hafla ya kutia saini makubaliano hayo Jijini Mwanza, Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa TASHICO Eric Hamissi alitaja amakubaliano hayo kuwa hatua muhimu ya kubuni uwezo wa majini wa kitaifa na kupanua jukumu la Tanzania la kuwa kitovu cha kibiashara.
“Ushirikiano huu umetekelezwa kutokana na mahitaji ya pande mbili. Tunataka kuboresha ufanisi kwatika uchukuzi wa majini na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika eneo la ziwa Tanganyika,” alisema Hamissi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya LMC ya DRC, Frank Nkulu alisema, uhusiano huo wa kampuni hizo mbili, utafanya mifumo ya usafiri wa majini kuwa ya kisasa na kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa jamii zinazozunguka Ziwa Tanganyika.
Aidha, wafanyabiashara walikaribisha hatua hiyo, wakisema itapunguza gharama na muda wa utoaji huduma na hivyo kufanikisha ukuaji wa biashara katika kanda hiyo.