Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mwenzake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, wamezindua ushirikiano mpya wa nishati baada ya kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuendeleza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta na Kitovu cha Nishati cha Kikanda mjini Tanga.
Mradi huo unaotarajiwa kuimarisha sekta ya nishati na uchumi wa katika kanda ya Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yalisainiwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na kampuni ya VTTO Bahrain, yakifungua njia ya maandalizi ya kitaalamu na uwekezaji wa ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
“Ushirikiano huu utaimarisha usalama wa nishati katika kanda hii, ukuaji wa viwanda na biashara. Kiwanda cha Tanga pamoja ni kile cha usafishaji mafuta cha Hoima nchini Uganda, vitahakikisha rasilimali za mafuta zinapata dhamani kubwa kupitia usafishaji, uhifadhi na uzalishaji badala ya kuagiza mali ghafi,” alisema Museveni.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk. Ruth Nankabirwa Ssentamu, alisema makubaliano hayo yanaonesha dhamira ya nchi hizo mbili ya kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta badala ya kuuza malighafi pekee.
Alisisitiza kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta kinachotarajiwa kujengwa Kabaale nchini Uganda na Kitovu cha Nishati cha Tanga havitakuwa washindani, bali vitasaidiana kuongeza uwezo wa usafishaji wa mafuta na kuimarisha upatikanaji wa nishati katika Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratias Ndejembi, alisema hatua hiyo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati.
Alieleza kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa za petroli, huduma za usafirishaji pamoja na bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta litakaloweza kufanya kazi kwa pande zote mbili kati ya Tanzania na Uganda.
Utiaji saini wa makubaliano hayo unaongeza hatua mpya katika ushirikiano wa muda mrefu wa Tanzania na Uganda kwenye sekta ya nishati, ulioanza kuimarika kupitia utekelezaji wa mradi wa EACOP mwaka 2017.