Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ameelezea kuwaunga mkono wakulima wa miwa nchini kwa kupinga mabadiliko kwenye sheria za sekta ya sukari, akisema Bunge la Taifa litalinda mageuzi yanayowawezesha wakulima na kufufua sekta hiyo.
Akizungumza alipokutana na viongozi wa Chama cha Kitaifa cha Wakulima wa Miwa (KNFSF), likiongozwa na mwenyekiti Ezra Okoth na Katibu Mkuu Kilion Osur katika majengo ya bunge, Spika huyo pia alitoa changamoto kwa wakulima hao kuongeza kampeni yao dhidi ya uagizaji sukari kutoka nje, ambao huenda ukahatarisha hatua zilizopigwa za kufufua sekta ya sukari nchini.
Chama hicho kilitoa wito kwa bunge kutupilia mbali marekebisho ya Mswada wa Sheria za Mimea mwaka 2026, akisema mabadiliko hayo yatadhoofisha uwakilishi wa wakulima na kuwanyima wakuzaji mimea udhibiti wa taasisi zilizobuniwa kulinda maslahi yao.
Katibu Mkuu wa chama hicho cha wakuzaji wa miwa Kilion Osur, alisema swala kuu la chama hicho ni pendekezo la kuondoa uchaguzi wa wakurugenzi na badala yake wateuliwe.
“Sheria ya sukari ni bayana kwamba wakurugenzi wa wakulima wanapaswa kuchaguliwa na wakulima. Hatutakubali mfumo ambapo wanateuliwa,” alisema Osur.
Hata hivyo alisema wamesuluhisha swala hilo na Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, ambapo pande zote mbili zilikubaliana Uchaguzi wa wawakilishi wa wakuzaji miwa kwenye Bodi ya Sukari ya Kenya utaendelea.
Akijibu maswala hayo ya wakulima, Wetang’ula alisema sheria ya sasa ya sukari inaashiria lengo la bunge na lilitiwa saini na Rais William Ruto bila mabadiliko.