Serikali inapoimarisha mfumo wa dijitali katika operesheni zake, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema mikakati imewekwa kulainisha usimamizi wa magari rasmi ya serikali kidijitali, ili kuleta uwazi na kuepusha matumizi mabaya ya fedha za umma.
Katika mkutano wa mashauriano na wawakilishi wa Serikali Kuu, bunge, Idara ya Mahakama pamoja na mashirika ya kiusalama, Koskei alisema mkutano huo uliangazia kurejelewa kwa taratibu za usimamizi wa magari yanayomilikiwa na serikali na kuziwianisha na mahitaji ya usafiri, maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya uwajibikaji yanayokua.
“Matumizi mabaya ya nambari za usajili wa magari ya serikali, changamoto kwa uwekaji rekodi za mafuta na umbali wa safari na ukosefu wa uwajibikaji kwenye magari yaliyotolewa na wafadhili baada ya kukamilika kwa miradi, unahujumu uwajibikaji katika utumishi wa umma,” alisema Koskei.
Kulingana na Koskei, kila shilingi inayotumiwa kuweka gari mafuta, bima, ukarabati au ununuzi wa magari megine, ni sharti ipige jeki utoaji huduma kwa kila mwananchi.
Serikali pia inakusanya hifadhideta ya kina kuhusiana na magari yake. Habari kutoka wizara mbalimbali, idara za serikali, mashirika na serikali za magatuzi zitathibitishwa ili kuandaa rekodi moja kuu huku hatua za salama zikiwekwa ili kuhakikisha uwajibikaji katika ughughulikaji wa deta, uwazi pamoja na usalama wa mitandaoni.
“Teknolojia peke yake haiwezi hakikisha uwajibikaji. Maafisa wa umma wanaojukumiwa na magari ya serikali lazima wawajibike kikamilifu, wadumishe nidhamu na wahakikish rasilimali hizo zinawahudumia wananchi,” aliongeza Mkuu huyo wa Utumishi wa Umma.
Alidokeza kuwa serikali itaendelea kutumia teknolojia kwa usimamizi, kutambua utumizi mbaya na kuimarisha uwajibikaji kwa mali ya umma.
Miongoni mwa wale waliohudhuria mkutano huo ni Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Amos Gathecha.