Nairobi yaanzisha ada mpya za vibali vya Kelele

Zinahusisha shughuli kama harusi, misafara ya matangazo, ujenzi, ibada za kidini, vilabu na matukio ya usiku ya muda mfupi.

Marion Bosire
2 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Waandaaji wa matukio, wafanyabiashara na taasisi jijini Nairobi sasa watalazimika kulipa ada mpya kwa shughuli zinazozalisha kelele chini ya Sheria ya Fedha ya Kaunti ya Nairobi ya mwaka 2026.

Ada hizo zinahusisha shughuli mbalimbali, kuanzia harusi na misafara ya matangazo hadi ujenzi, ibada za kidini, vilabu na matukio ya usiku ya muda mfupi.

Matukio ya usiku ya muda mfupi yatatozwa ada ya Ksh100,000, huku vilabu vikitozwa ada ya kila mwaka ya kati ya shilingi 20,000 na 100,000, kulingana na idadi ya watu vinavyoweza kuhudumia.

Kwa harusi, waandaaji watalipa shilingi 20,000 ikiwa sherehe itafanyika katika maeneo ya makazi na 10,000 kwa matukio yatakayofanyika kwenye bustani.

Gharama za misafara ya matangazo zitatofautiana kulingana na aina ya gari, kuanzia shilingi 10,000 kwa gari dogo hadi 50,000 kwa lori la magurudumu 24 au canter.

Shughuli za ujenzi zinazohusisha uchimbaji, ubomoaji na uchimbaji kwa mashine zitahitaji kibali cha shilingi 20,000. Makanisa na misikiti watalipa shilingi 5,000 kila mwaka kwa Kibali cha Kudhibiti Utoaji wa Kelele.

Hatua hizo zimekuja wakati wasiwasi kuhusu uchafuzi wa kelele jijini Nairobi unaongezeka. Kesi tofauti katika Mahakama Kuu inapinga matumizi ya muziki wa sauti kubwa katika magari ya usafiri wa umma.

Chini ya sheria hizo, ukiukaji wa masharti ya vibali unaweza kusababisha faini ya hadi mara tatu ya ada husika.

Share This Article