Uwasilishaji pesa kwa njia ya simu waongoza katika visa vya ulaghai

Uchunguzi umebaini kuwa huduma hizo zilitumika kuwasilisha fedha katika nusu ya visa vya ulaghai wa kompyuta kati ya Februari na Julai 2026.

Marion Bosire
2 Min Read
Raymond Omollo - Katibu wa Usalama wa Taifa.

Huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu imemulikwa huku serikali ikiongeza hatua za kupambana na uovu huo.

Katika taarifa, Wizara ya usalama wa ndani ilielezea kwamba uchunguzi umebaini kuwa huduma za pesa za simu zilitumika kama njia ya kuwasilisha fedha katika nusu ya kesi za utapeli wa kompyuta zilizoripotiwa kati ya Februari na Julai 2026.

Kamati ya kitaifa ya kuratibu masuala ya kompyuta na uhalifu wa mtandaoni ilisema kati ya visa 102 vya ulaghai wa fedha 51 vilitekelezwa kupitia huduma hiyo ya kuwasilisha pesa kwa njia ya simu.

Mpango huo umetajwa kuwa mkubwa zaidi wa utapeli kwa asilimia 18.6.

Utapeli wa uwekezaji na biashara ya fedha za kigeni ulifikia asilimia 15.7, huku ulaghai wa sarafu za kidijitali ukichangia asilimia 11.8.

Visa vya ulaghai viliongezeka kwa kasi kuanzia Mei, huku kesi 70 vikiripotiwa kati ya Mei na Julai. Julai ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya visa kwa mwezi, vikiwa 27.

Akizungumza katika mkutano wa 36 wa Kamati ya kitaifa ya kuratibu masuala ya kompyuta na uhalifu wa mtandaoni, Katibu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa Raymond Omollo, alitoa wito wa kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa miamala hatarishi ya pesa za simu, kuhifadhi ushahidi kwa haraka na kuimarisha ushirikiano na kampuni za mawasiliano.

Serikali pia inawaonya walaghai kuwa malalamiko yatachunguzwa na wahalifu watafikishwa mahakamani.

Wakenya wanahimizwa kutotoa nambari zao za siri yaani PIN, nywila au misimbo ya matumizi ya mara moja yaani OTP, na kutumia uthibitishaji wa hatua nyingi.

Umma pia ulielekezwa kuripoti mara moja miamala, nambari za simu, tovuti na akaunti zinazotia shaka.

Wakati huo huo matukio bilioni 2.3 ya uhalifu wa mtandaoni yaliripotiwa katika robo hiyo, ikiwa ni punguzo la asilimia 30 ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia.

Share This Article