Kesi iliyokuwa ikimkabili mwanamuziki, mwanamitandao na sasa mbunge wa Kigoma Mjini Clayton Revocatus Chipando, maarufu kama Baba Levo imefutiliwa mbali.
Watu wanne waliojitambulisha kama wapiga kura katika eneo husika, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu, walikuwa wamewasilisha kesi mahakamani kupinga kuchaguliwa kwa Baba Levo kama mbunge.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma leo Alhamisi Julai 16, 2026 imefuta kesi hiyo ya uchaguzi.
Katika uamuzi aliosomwa mahakamani leo, Jaji Victoria Nongwa aliyesikiliza kesi hiyo ya kupinga uhalali wa Ubunge wa Baba Levo amesema hoja zote zilizoletwa na walalamikaji ikiwemo hoja za utekaji, madai ya rushwa, udini na nyingine, hazikushawishi Mahakama moja kwa moja.
Jaji huyo alikubaliana na upande wa utetezi kwamba ushahidi uliowasilishwa Mahakamani ulikosa mashiko katika kesi hiyo nambari 28949 ya mwaka 2025.
Mahakama imesema dosari kadhaa zilibainishwa kwa upande wa walalamikaji ambao ni wanachama wa ACT Wazalendo na kwamba walalamikiwa wote ikiwemo tume ya uchaguzi hawana kesi ya kujibu.
Levo aliyekuwa amejawa na furaha pamoja na wafuasi wake walionekana wakicheza na kuimba nje ya mahakama huku akimahisi wakili wake zawadi ya gari aina ya Toyota Harrier.