Mgonjwa wa mwisho wa Ebola nchini Uganda ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupona kabisa katika Hospitali ya Kitaifa ya Rufaa.
Waziri wa Afya, Dkt. Chris Baryomunsi, alimkabidhi cheti cha kuruhusiwa kutoka hospitalini, akielezea kupona kwake kama hatua muhimu katika juhudi za Uganda za kudhibiti mlipuko huo.
“Hii inathibitisha kwamba kufikia Julai 2026, mtu huyo aliyepona hawezi kuambukiza watu wengine baada ya vipimo kuonyesha hana virusi vya Ebola,” alisema Dkt. Baryomunsi.
Aliongeza kusema kuwa hali ya afya ya mtu huyo sio tishio tena kwa jamii na kwamba anaweza kurejea nyumbani na kuendelea na shughuli zake za kila siku.
Tangu mlipuko huo ulipoanza mwezi Mei, Uganda imeimarisha juhudi za kinga, ikiwa ni pamoja na kudhibiti kutangamana kwa watu katika maeneo yanayopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kuzingatia karantini ya lazima kwa wasafiri wanaotoka Congo, na kuendesha kampeni kubwa za uhamasishaji wa umma kuhusu kinga dhidi ya Ebola.
Uganda imethibitisha kuwa watu 20 waligunduliwa kuwa na ugonjwa Ebola, viwili kati yao walifariki dunia lakini 18 wametibiwa na kupona.
Kulingana na Wizara ya Afya ya nchi hiyo, watu 15 kati ya wale waliopatikana na maambukizi ya ugonjwa huo walitokea DR Congo .
Mkuu wa Kituo cha Habari cha Serikali ya Uganda, Allan Kasujja, alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa X: “Siku 42 zikitapita bila visa vipya vya maambukizi, miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inaelekeza kuwa tutatangazwa kuwa huru dhidi ya Ebola.”
Taarifa ya BBC