Mwili wa Omar Seseme kuzikwa leo jioni

Seseme alifariki jana Mei 12, 2025 jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwili wa mwanamuziki mkongwe wa Tanzania Omar Seseme utazikwa leo jioni kuanzia saa kumi katika makaburi ya Mwinyimkuu, Magomeni Mapipa, karibu na Masjid Noor.

Haya ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA ambalo lilitangaza kifo chake kilichotokea jana Mei 12, 2025 jijini Dar es Salaam.

Marehemu Seseme anafahamika sana kwa uhusika wake katika muziki wa densi katika bendi mbali mbali ambapo alicheza gitaa ya Solo kwa ustadi mkubwa.

Omar Seseme alihudumu katika bendi nyingi maarufu nchini Tanzania kama vile African Revolution au Tam Tam, Double M Sound, Mchinga Generation, Wazee Sugu na Super Kamanyola ya Mwanza.

Bendi ya mwisho ambayo alihudumia ni Sikinde OG na alikuwepo hadi alipoanza kuugua baada ya onyesho lao la Machi 31, katika eneo la Brake Point Makumbusho.

Nyimbo za bendi ya Sikinde OG ambazo alichezea gitaa yake ya solo ni pamoja na Mchepuko, Hila za Ndugu, Moyo na Tonge la Mwisho.

“Tunatoa pole kwa familia, wanamuziki wenzake na wote walioguswa na msiba huu. Sanaa ya Tanzania imempoteza mmoja wa waasisi wake muhimu” ilisema taarifa ya BASATA.

Website |  + posts
Share This Article