Takriban familia 750 zenye mahitaji makubwa zinazotunza watoto mayatima na walio katika mazingira hatarishi katika Kaunti ya Isiolo zimepokea usaidizi mkubwa wa kiuchumi.
Hii ni baada ya kugawiwa shilingi milioni 104 kusaidia kujikimu kimaisha.
Mpango huo unaojulikana kama ‘Graduating Generations’, unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Catholic Relief Services kupitia CARITAS na Serikali ya Kaunti ya Isiolo, ukilenga wakazi wa wadi za Oldonyiro, Chari na Bulapesa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mpango huo mjini Isiolo, Mkurugenzi wa Catholic Relief Services Kenya Margaret Kahiga na Naibu Gavana wa Isiolo Dkt. James Lowasa walisema unalenga kuimarisha uwezo wa familia kujitegemea kiuchumi kupitia uwekezaji wa biashara, ujumuishaji wa kifedha, ulinzi wa kijamii na mafunzo ya ujasiriamali.
Kahiga alisema familia zote 750 zilizotambuliwa kwa kutumia taarifa kutoka kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame, NDMA na idara za serikali tayari zimepokea ruzuku ya kwanza ya shilingi 24,000 kila moja ili kuanzisha biashara ndogo wanazochagua.
Wanufaika watapatiwa mwongozo na wakufunzi wa biashara vijijini kwao, katika muda wa miezi 18 ili kusaidia biashara zao kukua na kuwa endelevu.
Familia zitakazofanikiwa kukuza biashara zao pia zitapatiwa nyongeza ya shilingi 5,000 katika nyakati ngumu kama misimu ya ukame ili kulinda mtaji wao.
Dkt. Lowasa alisema serikali ya kaunti itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa wanufaika hata baada ya muda wa mradi kukamilika.
Baadhi ya wanufaika, akiwemo Sabina Akiru na Caroline Njeri, wamepongeza mpango huo wakisema umerejesha heshima yao kwa kuwawezesha kukidhi mahitaji ya familia zao bila kutegemea msaada kutoka kwa majirani.