Wanasiasa wametakiwa kujiepusha na siasa za mapema na kuelekeza shabaha yao kwa ajenda ya maendeleo yanayotekelezwa na serikali kila sehemu ya nchi badala ya kuzamia siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Naibu Rais Kithure Kindiki amesema kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuharakisha miradi ya maendeleo na kuboresha huduma zinazotolewa kwa raia kote nchini.
“Nina furaha sana kumuunga mkono Rais katika uendeshaji wa nchi hii kwa sababu kwa mara ya kwanza katika kila kaunti, kila sehemu ya nchi tuna miradi mikubwa ambayo tunaweza kuzungumzia: barabara, umeme, maji, masoko, nyumba za gharama nafuu na mingine mingi,” alisema Naibu Rais.
“Haikuwa hivyo kabla. Kwa mara ya kwanza, kuna jitihada za kimakusudi za kuhakikisha kila sehemu ya nchi inafikiwa.”
Kindiki aliyasema hayo baada ya kukutana na viongozi kutoka kaunti ya Nandi wakiongozwa na Gavana Stephen Sang.
Mkutano huo ulipitia upya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika kaunti ya Nandi.
Viongozi hao walikubaliana juu ya hatua za kuharakisha utekelezaji na uimarishaji wa uangalizi wa miradi hiyo, na kuhakikisha ubora wa kazi inayofanywa na wanakandarasi.