Mwanamuziki wa Uganda Lil Pazo ametoa maoni yake kuhusu onyesho la hivi karibuni la Joshua Baraka katika tamasha ya Afro Nation iliyofanyika nchini Ureno.
Pazo ambaye jina lake halisi ni Yasin Mukasa, anasema msanii huyo mchanga anapaswa kuzingatia zaidi kujenga soko la muziki wake ndani ya Uganda kabla ya kulenga hadhira ya kimataifa.
Akizungumza katika mahojiano Lil Pazo alidai kuwa Baraka alipangiwa muda wa mchana kutumbuiza wakati ambapo wengi wa wahudhuriaji tamasha walikuwa bado hawajafika.
“Walimuweka aimbe mchana wakati watu wengi walikuwa bado hawajafika. Anapaswa kurudi nyumbani na kufanya muziki kwa ajili ya mashabiki wa hapa wanaoufurahia. Anapaswa kurudi kwenye uwanja na kufanya muziki pamoja na sisi,” alisema Pazo.
Hali hiyo kulingana na Pazo, iliwatia aibu Waganda na wasanii wa Uganda, walioko nyumbani na wale walio nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Lil Pazo, Joshua Baraka anapaswa kuweka kipaumbele katika kujenga msingi mkubwa wa mashabiki nchini Uganda badala ya kuelekeza nguvu nyingi kwenye maonyesho ya kimataifa.
Kauli za Lil Pazo zimeibuka wakati kuna mjadala kuhusu iwapo wasanii wa Uganda wanapaswa kwanza kujenga umaarufu mkubwa katika soko la ndani kabla ya kutafuta kutambulika kimataifa.
Tamasha ya Afro Nation iliandaliwa Julai 3 hadi 5 2026 katika ufukwe wa Praia da Rocha, jijini Portimão nchini Portugal.