Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Kenya Colonel Mustafa amehusishwa katika wimbo mpya uitwao “Palm Tree” ambao umetolewa kwenye YouTube siku mbili zilizopita.
Wimbo huo umeandikwa na mwanamuziki Mikal Aaron ambaye ameuimba huku akimhusisha Mustafa.
Unahusu mapenzi ambapo katika ubeti wake, Mustafa anakiri kwamba hajamwona mpenzi wake kwa muda mrefu na angependa kumwona huku akimsihi achukue simu ili wawasiliane.
Katika pambio, Mikal anamjibu kwamba iwapo anataka kumwona atampata karibu na mtende au ukipenda mnazi.
Msanii huyo anaonekana kurejelea kikamilifu kazi yake ya muziki baada ya kupitia matatizo si haba katika miaka ya hivi karibuni.
Mwezi Mei mwaka 2023, msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Daud Mustafa alijitokeza kuomba msaada kutoka kwa wakenya akielezea kwamba mamake alikuwa akiugua saratani na matibabu yalikuwa ghali.
Ilibainika kwamba alikuwa na matatizo ya kifedha wakati akijaribu kumtunza mamake na akiendelea kujenga lakini wakenya walijitokeza na kumsaidia.
Tangu wakati huo ameonekana kunawiri ambapo amehudhuria tamasha kadhaa na kufanya matangazo ya kibiashara, kama njia ya kujipatia kipato.