Saa chache baada ya mkewe kutangaza kuvunjika kwa ndoa yao ya miaka 7, mwigizaji maarufu nchini Martin Githinji maarufu kama Daddie Marto amekanusha madai yake kwamba alimshambulia.
Christine Koku Lwanga alitumia Insta Stories kufichua habari hizo ambapo aliziambatanisha na picha zao za pamoja ambapo alisema kwamba Marto alimshambulia alipomfumania na mwanamke mwingine.
Kulingana naye, baba huyo wa watoto wake alikodisha nyumba nyingine karibu na wanakoishi akiirejelea kuwa afisi lakini akawa anaitumia pamoja na mwanamke huyo mwingine.
Sasa Marto ametoa taarifa rasmi ambapo anakanusha taarifa alizosambaza Koku akisema yeye huwa hakubaliani na vurugu na kwamba alitumai kusuluhisha matatizo ya ndoa yake kimya kimya lakini sasa yameletwa mitandaoni na analazimika kujibu.
“Tumaini langu la msingi lilikuwa kusuluhisha maswala haya kwa faragha ili kuhakikisha usalama wa wanangu na wahusika wote lakini hali ya ufichuzi mitandaoni inanilazimisha nijibu hadharani,” alisema mwigizaji huyo katika taarifa yake.
Aliendelea kusema kwamba huwa hakubaliani na vurugu za aina yoyote huku akimlaumu Koku kwa kutoelezea kikamilifu kuhusu yaliyotokea na muktadha halisi.
“Kinachoenezwa kwa sasa sio tu cha kupotosha bali pia ni cha kuharibu pakubwa kwangu, kwa wanangu, familia zetu na jamii tunazoishi,” Alielezea Marto.
Huku akidai kwamba ana ushahidi wa hali halisi, Marto amesema kwamba ataruhusu njia mwafaka za kusuluhisha matatizo yao ifaavyo badala ya mivutano mitandaoni.
Amesema anashirikiana kikamilifu na asasi za kisheria na ametafuta pia usaidizi wa kisheria ili kuhakikisha usalama wake na wa wahusika wote.
Mwigizaji huyo amekiri kwamba utengano sio rahisi hasa wakati watoto wako lakini ameahidi wanawe kwamba atakuwa nao kila wakati na atakuwa mkweli kwao.