Wolper mmoja wa majaji katika shindano la wataalamu wa kupaka vipodozi

Kipindi hicho kilichopatiwa jina la "The Makeover Show" kitapeperushwa kwenye Maisha Magic Bongo kuanzia Ijumaa wiki ijayo.

Marion Bosire
1 Min Read
Jackline Wolper

Mwigizaji wa muda mrefu na mwanabiashara wa Tanzania Jackline Wolper ni mmoja wa majaji katika shindano la wataalamu wa mapodozi ambalo litakuwa kipindi kitakachopeperushwa na Maisha Magic Bongo.

Kupitia akaunti yake ya Instagram Wolper alitoa tangazo hilo ambapo alichapisha picha ya pamoja na majaji wenzake katika kipindi hicho kitakachoanza rasmi Aprili 25, 2025 saa mbili usiku.

Amerejelea shindano hilo kuwa “Kabumbu ya Brush na Powder” akisema yeye amekuwa kwenye tasnia ya urembo na vipodozi kwa muda mrefu.

Kulingana na matangazo kwenye akaunti rasmi ya Instagram ya kipindi hicho kilichopatiwa jina la “The Makeover Show” walianza kwa kualika wanaotaka kushiriki na ambao ni wataalamu wa mapodozi yaani ‘Makeup Artists’.

Tangazo la wito lilitolewa Januari 30 ambapo walihitajika kutuma video za dakika moja zinazoonyesha kazi zao za kupaka wateja wao vipodozi huku tarehe ya mwisho ikiwa Februari 6, 2025.

Inaonekana kwamba wameshafanya mchujo na kuchagua watakaoanza kipindi hicho cha kwanza cha aina yake nchini Tanzania.

Majaji wengine katika kipindi hicho ni Martin Kadinda na Alma Aboubakar Omar Salum maarufu kama Almah Bronxi huku mtangazaji anayejihusisha na masuala ya mitindo ya mavazi Annie Independent akikiongoza.

Website |  + posts
Share This Article