Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), umetangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 ulishindwa kukidhi viwango vya kidemokrasia vya jumuiya hiyo.
Kulingana na SADC, uchaguzi huo ulikumbwa na vitisho vya viongozi wa upinzani, vikwazo vya uhuru na ukosefu wa uwazi wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.
Katika taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari, shirika hilo limesema ingawa siku ya upigaji kura kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya amani, “katika maeneo mengi, wapiga kura hawakuweza kueleza kwa uhuru mapenzi yao ya kidemokrasia.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa uchaguzi huo “ulipungukiwa na matakwa ya Kanuni na Miongozo ya SADC ya Kusimamia Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021)”, kigezo cha uchaguzi huru, wa haki, na wa kuaminika miongoni mwa nchi wanachama.
Ujumbe huo vilevile uliripoti kuhusu kutengwa kwa wagombea wa upinzani kwa kukamatwa, na kupewa vitisho – ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa kiongozi wa upinzani Tundu Lissu kwa tuhuma za uhaini.
SADC imesema vitendo hivi vinadhoofisha demokrasia ya vyama vingi vya Tanzania na kukatisha tamaa ushiriki wa wapiga kura.