Rais William Ruto ametangaza kwamba amefanya tamasha ya kitaifa ya washindi wa mashindano ya shule na taasisi ya uigizaji na filamu kuwa hafla ya kitaifa.
Akizungumza katika Ikulu ndogo ya Nakuru wakati wa awamu ya 63 ya tamasha hiyo ya kila mwaka, Kiongozi wa taifa alisema serikali imejitolea kuhakikisha ustawi wa uchumi wa ubunifu nchini.
Rais Ruto alisifia wajibu unaotekelezwa na sanaa katika kuunda utambuzi wa taifa, kukuza maadili na kuunda fursa za kiuchumi. Alipongeza maigizo ya leo kwa kuonyesha uzalendo, umoja, hadhi na haki ya kijamii.
“Tamasha hii sio tu ya kusherehekea ubunifu, ni jukwaa la kitaifa la kujieleza, kukuza talanta na kuhifadhi tamaduni zetu.” Alisema Rais akiongeza kwamba hawaungi sanaa mkono kimfano tu bali wanaiunga mkono kimkakati.
Aliangazia mipango ya serikali ya kusaidia sekta ya ubunifu kama vile kuwekwa kwa hifadhi za kidijitali kwa maigizo ya awali, ufadhili zaidi kupitia kwa tuzo za uigizaji za Kenya na mipango ya kujenga studio za kitaifa za filamu.
Rais alisifia mpango wa Talanta Hela ambao umetoa ufadhili wa masomo kwa waigizaji stadi wa umri mdogo.
Katika kutambua wasanii waanzilishi, Rais alitaja mashujaa kama Profesa Francis Imbuga, John Sibi-Okumu, Oliver Litondo na mwigizaji wa Hollywood wa asili ya Kenya Edi Gathegi, akiwataja kuwa mabalozi wa sanaa na utamaduni wa Kenya.
Kiongozi wa nchi alimalizia kwa kuwasihi wakenya waishie maadili waliyoonyesha jukwaani akisema, “Taifa linalotambua wasanii wake ni taifa ambalo linathamini moyo wake”.