Aliyekuwa mbunge wa Mathioya akamatwa kwa ulaghai wa ardhi

Tom Mathinji
1 Min Read
Mbunge wa zamani wa Mathioya Francis Njakwe Githiari,.

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, wamemkamata aliyekuwa mbunge wa Mathioya Francis Njakwe Githiari, kwa madai ya kuwalaghai wanandoa shilingi milioni 6.4 kwenye sakata ya ardhi.

Wanandoa hao walitia saini mkataba na Githiari ili kununua kipande cha ardhi katika eneo la Ngong, ambapo walilenga kujenga jumba la gorofa mbili.

Githiari, ambaye alijisingizia kuwa mkandarasi, alikuwa na jukumu la kuuza na kujenga jumba hilo.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema gharama ya ardhi hiyo na ujenzi wa jumba hilo, ilikuwa shilingi  milioni 40 million, zilizokuwa zilipwe kwa awamu.

Hata hivyo, wakati wanandoa hao walipokuwa wakizuru eneo hilo, waligundua ardhi hiyo ilidaiwa kumilikiwa na watu wengine.

“Uchunguzi ulianzishwa na maafisa wa DCI, uliobainisha kuwa Githiari alipokea fedha kutoka kwa wanandoa hao kwa njia za ulaghai,” ilisema taarifa ya DCI.

Kwa sasa Githiari  anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Karen, akitarajiwa kufikishwa mahakamani Ijumaa Mei 15, 2026.

Share This Article