Watu kadhaa wamefariki na wengine kujeruhiwa, baada ya mwanafunzi kuwashambuliwa kwa risasi katika shule moja ya Upili Jijini Bangkok,Thailand.
Shambulizi hilo la risasi la Ijumaa asubuhi, lilitekelezwa katika shule ya Debsirin Nonthaburi, katika mkoa wa Nonthaburi muda mfupi baada ya saa nne asubuhi saa za nchi hiyo.
Huku idadi kamili ya waliofariki ikikosa kubainika, Waziri wa Afya wa nchi hiyo Pattana Promphat, amesema watu 22 wamejeruhiwa, tisa kati yao wakiwa hali mahututi.
Duru zinasema kuwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 14, aliwafyetulia risasi walimu na wanafunzi kabla ya kujitoa uhai.
Kulingana na walioshuhudia shambulizi hilo, wanafunzi walijificha ndani ya madarasa yao waliposikia milio ya risasi, kabla ya maafisa wa polisi kuwaokoa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Polapee Suwunchwee, aliwaambia wanahabari kuwa mwanafunzi huyo aliwaua babu na nyanya yake kwanza, kabla ya kuelekea shuleni kutekeleza shambulizi hilo.
Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul, ametuma rambirambi zake, huku akitoa agizo kwa maafisa husika kuwashughulikia ipasavyo waathiriwa.