Timu ya Kenya katika soka ya wanawake, Harambee Starlets ilianza vibaya ushiriki wake katika kipute cha Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON ), baada ya kulabuliwa magoli manne bila jawabu na wenyeji Morocco katika mchuano wa kundi A uliosakatwa katika uchanjaa wa Prince Moulay Hassan jijini Rabat Jumapili usiku.
Sakina Ouzraoui, Maryame Atiq na Ibtissam Jraidi walitikisa nyavu kila mmoja katika kipindi cha kwanza huku Starlets wakitota kuelekea mapumzikoni wakiwa nyuma mabao matatu kwa nunge.
Mbinu za kocha Beldine Odemba za kujaribu kuwasakama wenyeji kwa mashambulizi ya kushtukiza ziliwapa wapinzani fursa si haba kunako kipindi cha kwanza za kushambulia na hata kufunga mabao.
Hata hivyo, Odemba alibadili mbinu katika kipindi cha pili na kuziba mianya ya wazi waliyokuwa wakiacha nyuma wakati wa kushambulia ingawa hawakufua dafu kuwadokoa wenyeji.

Jraidi alitanua uongozi wa Atlas Lionesses kwa goli la nne dakika mbili tu baada ya mapumziko.
Kutoka hapo, mchezo ulisalia kuwa mazeozi tu hadi kipenga cha mwisho Kenya wakibuni nafasi tatu ila mabeki wa Morocco na kipa walikaa ange na kuwazima.
Starlets watarejea uwanjani dhidi ya Senegal waliopigwa 2-0 na Algeria katika mchuano wa ufunguzi Julai 30 katika mechi ya kufa kupona, kwani atakayeshindwa atafunganya virago.
Mataifa 16 yanashiriki patashika hiyo huku timu nne bora zikifuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Brazil.